Email:info@zyc.go.tz
   

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Baraza la Vijana Zanzibar

Mawasiliano - Baraza la Vijana Zanzibar

Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Hassan Hafidh Ameir akifatilia zoezi la Uchaguzi Shehia za Unguja

News Image

Mwandishi: Bahati Habibu Peter

Tarehe: Monday, 23rd February 2026

Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Hassan HafidhAmeir, amewataka vijana kuchagua viongozi bora, waadilifu na wenye kujitambua ili kuimarisha maendeleo ya shehia zao na kulinda maslahi ya vijana.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea zoezi la uchaguzi wa Mabaraza ya Vijana katika Shehia ya Sebleni na kwa Wazee Wilaya ya Mjini, amesema viongozi watakaochaguliwa wanapaswa kujenga mashirikiano imara na vijana wenzao ili kuhakikisha mabaraza hayo yanafanya kazi kwa ufanisi.

Aidha, amewahimiza viongozi hao kuongoza kwa umahiri na kuepuka vitendo vya chuki, fitina na migogoro vinavyoweza kusababisha mfarakano miongoni mwa vijana.hao.

Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa Serikali imeanzisha Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji kwa lengo la kuimarisha maslahi ya vijana nchini kwa kuwawezesha kupata ajira katika sekta za umma na binafsi, pamoja na kuwapatia fursa za mikopo nafuu kwa ajili ya kujiajiri na kuajiri wengine.

Amesisitiza kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha vijana wa Zanzibar wanapata ajira na kipato halali kwa ajili ya kujikimu wao na familia zao, hatua itakayowasaidia kuepuka kujiingiza katika makundi maovu yanayodumaza maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana, Ndugu Ali Haji Hassan, amewataka vijana kudumisha umoja na mshikamano baada ya uchaguzi kukamilika ili kufikia maendeleo endelevu

Amesema Mabaraza ya Vijana ni jukwaa muhimu la kuibua na kuwasilisha changamoto zinazowakabili vijana pamoja na kupata suluhisho na fursa mbalimbali za maendeleo.

Nao baadhi ya vijana walioshiriki katika zoezi hilo wamesema watahakikisha wanaimarisha mabaraza hayo kwa kuwahamasisha wenzao kujiunga na kuyatumia kama chombo cha kuwasilisha changamoto zao.

Zoezi la uchaguzi wa Mabaraza ya Vijana ngazi ya shehia limefanyika leo katika mikoa mitatu ya Unguja, na linatarajiwa kuendelea kesho katika mikoa miwili ya Pemba.

Taarifa za Miradi