Email:info@zyc.go.tz
   

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Baraza la Vijana Zanzibar

Mawasiliano - Baraza la Vijana Zanzibar

Wahitimu wa Mafunzo ya Vijana Viongozi

News Image

Mwandishi: Bahati Habibu Peter

Tarehe: Tuesday, 10th June 2025

Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan ametoa wito kwa Wahitimu wa Mafunzo ya Vijana Viongozi kuyatumia mafunzo na Majukwaa ya Kimtandao katika kukuza na kupata fursa za masoko ya Biashara.

Akizungumza katika mahafali ya mwanzo ya Vijana Viongozi katika Ukumbi wa COSTECH uliopo Maruhubi Zanzibar amesema wakati umefika wa Vijana kutumia Mitandao kuwa ni fursa ya Kutangaza biashara wanazozifanya jambo litakalowasaidia kuongeza wateja na kujiongezea kipato.

Aidha amesema kwa sasa mitandao imechukua nafasi kubwa ya mawasiliano hivyo amewataka Vijana hao kutumia mafunzo walioyoyapata kwa kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kutumia Mitandao kukuza biashara na kutafuta masoko.

"Niwaambie Vijana Mafunzo haya mliopatiwa kwa muda wa siku kumi mnapaswa kuyatumia na kuwa mfano kwa Vijana wengine kwa Kuwa Viongozi bora katika jamii" Alisema Katibu Mtendaji huyo.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Pamoja Youth Initiative, Rashid Mwinyi amesema kupitia Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya Vijana wataendelea kuwasimamia Vijana ili kuwasaidia kufikia ndoto zao.

Pia amefahamisha kuwa Taasisi hiyo ipo tayari kushirikiana wadau mbalimbali katika kuhakikisha Vijana wanatumia Majukwaa ya Kimtandao Vizuri na sio kutumia majukwaa hayo kuwa chanzo cha kuharibu jamii hasa Vijana.

Kwa upande wa Mwakilishi wa Digital Opportunity Trust (DOT) Ndugu Edson Stanley amesema wamefarajika kuona Vijana hao wamemaliza vizuri mafunzo hayo na wana shauku kubwa ya kurudi katika jamii kuifikisha elimu waliopata.

Akitoa neno la Shukran kwa niaba ya Vijana Salmin Amour amesema kupitia mafunzo hayo walioyopata ni matarajio yao yataenda kuwa faraja kwao kwa kuwasaidia Vijana kukuza biashara na kutafuta biashara zao.

Mafunzo hayo ni utekelezaji wa mradi wa Going Beyond unaotekelezwa kwa mashirikiano baina ya taasisi ya Pamoja Youth Initiative, Digital Opportunity Trust na Mastercard Foundation yametolewa kwa muda wa siku kumi yametolewa kwa vijana wapatao 12 kutoka Unguja na Pemba

Taarifa za Miradi